Kanu atoa somo, amfagilia Samatta.
GWIJI wa soka wa zamani wa timu ya Taifa ya Nigeria `Super Eagles’ na klabu ya Arsenal ya England, Nwankwo Kanu amesema kwa sasa soka la Tanzania linajulikana baada ya mchezaji, Mbwana Samatta kusajiliwa na Klabu ya KRC Genk inayoshiri Ligi Kuu Ubelgiji.
Mbali ya Arsenal, nyota huyo amecheza pia klabu za West Brom na Portsmouth za England, Inter Milan ya Italia na Ajax Amsterdam ya Uholanzi aliyoisaidia kutwaa ubingwa wa Ulaya msimu wa 1994/95 akiwa kinda wa miaka 19 tu.
Kwa sasa Kanu ana umri wa miaka 39. Pia Kanu amesema ili soka la Tanzania liweze kukua na kuwa na wachezaji wengi zaidi watakaoweza kucheza soka la kulipwa barani Ulaya ni lazima izingatiwe uanzishwaji wa vituo vingi vya kulelea vipaji vya vijana.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akizindua duka jipya la Startimes lililopo katika Jengo la Mkuki, Kanu alisema awali alikuwa akilijua soka la Tanzania kwa kupitia timu ya taifa pale ilipokuwa inacheza mechi za kimataifa za kirafiki au za mashindano.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Tanzania, nimekuwa Kenya na Uganda, na nilikuwa nalijua soka la Tanzania kupitia timu ya taifa, lakini kwa sasa nalijua baada ya Mbwana Samatta kusajiliwa na Genk,” alisema Kanu.
Alisema ili Tanzania iwe na akina Samatta wengi katika soka la kulipwa Ulaya, inatakiwa kufanya jitihada za makusudi za kujenga msingi mzuri wa kukuza wachezaji vijana. “Naamini kama Tanzania itakuwa na vituo vingi vya kulelea vipaji vya wachezaji vijana, mtaweza kuwa na wachezaji wengi wa kulipwa Ulaya kama ilivyo kwetu Nigeria,” alisema.
Kanu alisema kuwa katika kupata wachezaji wengi hakuna njia ya mkato, ni lazima nchi ijitahidi kuzalisha na kukuza vipaji vingi vya wachezaji kama ilivyo katika nchi za Afrika Magharibi.
Kanu yupo nchini kwa ziara ya siku nne ukiwa ni mwaliko wa Startimes ambayo ni balozi wake na kesho atakuwa Mbagala Zakhem, ambako atakutana na wachezaji wadogo wa soka. Mbagala ni eneo alikokulia Samatta.
No comments:
Post a Comment