Rais Rousseff apigania kubakia madarakani.
Rais wa Brazil Dilma Rousseff hapo jana ameendelea na jitihada za kupigania kuendelea kubakia madarakani akifanya mikutano ya faragha muda mchache kabla ya upigaji kura baadaye hii leo utakaoamua iwapo kiongozi huyo atapelekwa katika bunge la Seneti ambako kesi dhidi yake inatarajiwa kufanyika. Rousseff ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke nchini humo ameshutumu kile alichoita mipango ya kutaka kumn'goa madarakani . Kiongozi huyo pia alifuta ratiba yake ya awali aliyopanga kukutana na makundi ya waandamanaji wanaomuunga mkono na badala yake kujikita katika kutafuta kuungwa mkono na wabunge nchini humo. Makamu wa Rais wa nchi hiyo Michel Temer ambaye sasa amegeuka kuwa hasimu wake na anayeongoza mapambano dhidi ya Rousseff naye pia aliondoka mjini Sao Paulo kurejea mjini Brasilia hatua ambayo vyombo vya habari nchini humo vimesema inaonyesha kuwepo ushindani mkubwa katika suala hilo. Upinzani nchini Brazil unahitaji kiasi ya kura 342 kati ya kura 513 au theruthi mbili kutoka katika bunge la wawakilishi ili kuamua kumfikisha Rais Rousseff katika seneti ambako kesi dhidi yake inaweza kufanyika.
No comments:
Post a Comment