Hofu yatanda kabla ya uchaguzi wa Rais Congo, Brazzaville.
Hofu imetanda katika Jamhuri ya Congo kabla ya uchaguzi wa Rais unaofanyika leo. Hii ni baada ya serikali kuziamuru kampuni zote za simu kusitisha huduma zao kwa sababu za kiusalama na polisi ikamwita mgombea mkuu wa upinzani ili kumhoji. Viongozi wa kisiasa wanasema amri ya kuzitaka kampuni za simu kukata mawasiliano itaathiri kazi ya waangalizi wa uchaguzi. Rais Denis Sassou Nguesso anatarajiwa kuurefusha utawala wake wa muda mrefu katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa kuwashinda wapinzani wanane, akiwemo Jenerali mstaafu Jean-Marie Mokoko ambaye anaonekana kuwa mpinzani mkubwa. Akizungumza akiwa nyumbani kwake Brazzaville, Mokoko alisema jana kuwa alitakiwa kufika katika makao makuu ya polisi kwa ajili ya kuhojiwa lakini akakataa kwenda. Sassou Nguesso ameiongoza Jamhuri ya Congo, kwa miaka 32 na akawezesha marekebisho ya katiba mwezi Oktoba kuondoa ukomo wa muhula na umri mambo ambayo yangemzuia kugombea tena.
No comments:
Post a Comment