Tuesday, March 15, 2016

Trump ashinda majimbo muhimu Marekani.


Donald Trump amepiga hatua katika kukaribia kutwaa tiketi ya kuwania urais kupitia chama cha Republican nchini Marekani baada ya kushinda mchujo majimbo matatu makubwa, likiwemo jimbo la Florida.
Bilionea huyo kutoka New York ameshinda majimbo ya Illinois na North Carolina.
Hata hivyo ameshindwa na John Kasich jimbo la Ohio.
Mgombea anayeongoza chama cha Democratic Hillary Clinton naye amepanua uongozi wake kwa kupata ushindi majimbo ya Florida, Ohio, Illinois na North Carolina.
Marco Rubio, mmoja wa waliotarajiwa kutoa ushindani kwa Trump katika chama cha Republican amejiondoa baada ya kushindwa na Trump katika jimbo lake la nyumbani la Florida.
Majimbo matano makubwa, Florida, Missouri, North Carolina, Ohio, Missouri na Illinois, yalifanya mchujo Jumanne.
"Lazima tuunganishe chama,” amesema Bw Trump akihutubu Palm Beach, Florida, baada ya kupata ushindi.
Anatumai kwamba ushindi huo utamfungulia njia ya kupeperusha bendera ya chama cha Republican.
John Kasich hata hivyo ameshinda jimbo lake la kwanza tangu mchujo kuanza, jimbo la Ohio ambako yeye ndiye gavana.
Akihutubu baada ya ushindi, Bw Kasich amesema anataka kuweka “mazingira ya kubuni nafasi” kwa vizazi vijavyo na pia akampongeza Bw Rubio kwa kampeni yake.
Bw Rubio ametangaza kujiondoa kwake kwenye kinyang’anyiro katika mkutano wa kampeni mjini Miami baada ya kushindwa Florida.
Amesema Marekani imo kwenye dhoruba ya kisiasa na kwamba wapiga kura wamekasirika na kutamauka.
Katika jiji hilo, Bi Clinton ametoa hotuba yake akifurahia ushindi ambapo amemshutumu Bw Trump na kusema „Wamarekani wana hamu ya kupata suluhu (kwa changamoto zinazowakabili)”.
Mpinzani wake, seneta wa Vermont Bernie Sanders, amewahakikishia wafuasi wake Phoenix, Arizona, kwamba atasalia kwenye kinyang’anyiro na kusema tayari kampeni yake imezidi matarajio ya wengi.
Majimbo ya Florida na Ohio huwa muhimu sana kwa chama cha Republican kwani mshindi hukabidhiwa wajumbe wote.
Florida huwa na wajumbe 99 na Ohio wajumbe 66.

No comments:

Post a Comment