Jukwaa laanguka Odinga akihutubu pwani ya Kenya.
Video inayoonesha kiongozi wa upinzani Kenya Bw Raila Odinga na viongozi wengine wakianguka baada ya jukwaa kuporomoka akihutubia mkutano wa hadhara imevuma sana mtandaoni Kenya.
Bw Odinga alikuwa akihutubu katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Malindi, jimbo la Kilifi katika pwani ya Kenya Alhamisi wiki iliyopita jukwaa lilipodondoka.
Mkutano huo ulikuwa wa kuwashukuru wapiga kura kwa kumpigia kura mgombea wa chama chake cha ODM Willy Mtengo kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Machi 7.
Bw Mtengo alishinda uchaguzi huo.
Ilikuwa siku moja kabla ya Ijumaa Kuu na Bw Odinga alikuwa akisimulia kuhusu mateso aliyopitia Yesu Kristo.
“Wakati huu mimi nilikuwa nimeenda kule Jericho, nikaonyeshwa ile mlima ya majaribio. Pale ambapo shetani alimpeleka Yesu akamuonesha ulimwengu wote. Akamwambia angalia hii yote. Ukikubali kusujudu na kuniabudu hii yote itakuwa ni yako. Lakini Yesu akamwambia wewe nenda mbali shetani ..” alisema Bw Odinga kabla ya jukwaa kuanguka.
Video hiyo imesambazwa sana mtandaoni.
Bw Odinga alikuwa ziarani Israel mapema mwezi huu.
Naibu mwenyekiti wa chama cha ODM eneo la Kilifi amenukuliwa na gazeti la Daily Nation la Kenya akisema hakuna aliyejeruhiwa kwenye kisa hicho.
Anasema watu waliokuwa kwenye jukwaa walipunguzwa na Bw Odinga akaendelea kuhutubia mkutano huo.
No comments:
Post a Comment