Magufuli: Wanafunzi waliofuzu ndio wapewe mikopo.
Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake itahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo,na kwamba serikali yake haitakubali kuelekeza mikopo hiyo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu.
Akiwahutubia maelfu ya wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wa chuo kikuu cha Dar es salaam, Dkt. Magufuli amesema serikali yake itatoa elimu bora kwa watanzania na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto mbalimbali zinazovikabili vyuo.
Katika taarifa ya ikulu ilotumwa kwa vyombo vya habari Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na uwepo wa wanafunzi waliodahiliwa na baadhi ya vyuo nchini pasipo kuwa na sifa zinazomwezesha mwanafunzi kujiunga na chuo kikuu.
Rais huyo ameyazungumza hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho inayojengwa katika kampasi ya Mlimani upande wa mashariki mwa chuo.
"Wapo wanaokopeshwa mikopo hii ya elimu ya juu lakini hawana sifa, Mheshimiwa Profesa Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi) nakushukuru kwa hatua unazozichukua katika kusafisha wizara yako na hili nalisema kwa uwazi, na ukweli lazima usemwe hata kama ni mbele ya wanachuo''.
"Una D,D unasajiliwa kuchukua digrii chuo kikuu na unapata mkopo wa serikali, ni aibu ya ajabu, haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani. Lakini wakati tunawalipia wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na kupata D,D manaake wengine ni divisheni 4, kuchukua digrii, wapo wanafunzi wengine wa kidato cha sita wamekosa mikopo, wapo wanafunzi wengine walio na diploma wamekosa mikopo" Amesema Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment