Tuesday, June 14, 2016

Mateen hakushawishiwa kufanya mauaji Orlando.


Image copyrightEPA
Image captionRais Obama amesema Mateen hakushawishiwa kutoka nje
Rais wa Marekani, Barack Obama amesema hakuna ushahidi kuwa aliyetekeleza mashambulizi kwenye klabu ya usiku mjini Orlando alikuwa sehemu ya mpango mkubwa wa mashambulizi.
Obama ameeleza shambulio hilo lilisukumwa na msimamo binafsi wa mshambuliaji huyo na hakuna ushahidi kuwa Omar Mateen alipata maelekezo kutoka nje kutekeleza mauaji.
Mkurugenzi wa shirika la kijasusi FBI,James Comey amesema kuna ishara kuwa Mateen alishawishika kupitia mitandao ya intaneti.Lakini amesema haijulikani Mateen alikuwa akiunga mkono kundi gani la kigaidi.
Comey amesema muuaji huyo alieleza kuunga mkono kundi la wanamgambo wa IS na hasimu wa kundi hilo, Al Nusra la nchini Syria.
Image copyrightAFP
Image captionTrump amepinga waislamu kuingia Marekani,jambo ambalo Hillary Clinton haliungi mkono
Mgombea Urais kwa tiketi ya Republican nchini Marekani, Donald Trump amerejea kauli yake akitaka kuwazuia kwa muda waislamu kuingia nchini Marekani.
Katika hotuba yake huko New Hampshire, Trump amesema mfumo wa Idara ya uhamiaji nchini Marekani umeruhusu familia ya Omar Mateen kuingia nchini Marekani huku akidai kuwa wauaji wengine wamendelea kuruhusiwa kuingia nchini humo
''Sababu pekee ya muuaji kuwepo nchini Marekani ni familia yake kuja hapa.huo ndio ukweli, ni ukweli unaopaswa kuzungumziwa.tuna mfumo wa idara ya uhamiaji isiyotekeleza wajibu wake,ambayo haituruhusu kujua ni nani tunaowaruhusu kuingia nchini mwetu na mfumo hauruhusu kuwalinda vyema raia wetu''
Akizungumza jimboni Ohio,Mgombea urais kupitia Chama cha Democratic, Hillary Clinton,amekosoa mpango wa mpinzani wake Donald Trump kuwazuia waislamu kuingia Marekani
''hatua hiyo ya uchochezi ya vitisho kuzuia familia na marafiki wa kiislamu kuingia marekani, pia mamilioni ya wafanya biashara na watalii waislamu kuingia nchini humo inaumiza sehemu kubwa ya waislamu wanaopenda uhuru na kuchukia ugaidi''.
Katika hatua nyingine,Silaha mbili kati ya zilizotumiwa na Mateen zilinunuliwa kwenye kituo cha kuuza silaha.Mmiliki wa duka hilo Edward Henson amesema Mateen alipitia taratibu zote zinazopaswa kupitia wakati wa kununua silaha.

No comments:

Post a Comment