Friday, May 6, 2016

Mfanyabiashara Jacob Juma auawa Nairobi


JumaImage copyrightFacebook
Image captionBw Juma alikuwa mkosoaji mkuu wa serikali
Mfanyabiashara mashuhuri Jacob Juma, ambaye amekuwa akizua mjadala mitandaoni Kenya kutokana na ujumbe wake anaoandika hasa kwenye Twitter, ameuawa kwa kupigwa risasi jijini Nairobi.
Taarifa zinasema Bw Juma alipigwa risasi na watu ambao walikuwa wakiendesha pikipiki alipokuwa akielekea nyumbani kwake mtaa wa Karen mwendo wa saa nne usiku.
Gari lake lilipatikana na zaidi ya matundu 10 ya risasi.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya, polisi wanasema hakuna kilichoibiwa kutoka kwenye gari lake. Simu zake mbili na pesa vilipatikana ndani ya gari.
Bw Juma alikuwa mwanakandarasi ambaye pia alihusika katika sekta ya uchimbaji madini.
Alikuwa mkurugenzi katika kampuni ya Erad iliyoshtaki Bodi ya Taifa la Nafaka na Mazao kuhusu kandarasi. Alitaka alipwe jumla ya Sh500m na bodi hiyo.
Agosti mwaka jana, alimshtaki Gavana wa jiji la Nairobi Dkt Evans Kidero akitaka akaunti zake za benki zifungiwe kwa tuhuma kwamba gavana huyo alihusika katika ufujaji pesa kampuni ya sukari ya Mumias Sugar.
Bw Juma pia alimshtaki waziri wa madini Najib Balala mwaka jana baada ya leseni ya kampuni yake ya madini ya Cortec Mining kupokonywa leseni.
Miaka 10 iliyopita, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, Bw Juma pia alimshtaki bintiye rais wa zamani Daniel arap Moi kuhusiana na shamba la ekari 250.
Aidha, aliwasilisha kesi mbili dhidi ya Naibu Rais William Ruto.

No comments:

Post a Comment