Mkanda wa video wamuumbua waziri Brazil
Waziri wa mipango katika serikali mpya ya Brazil anakaa pembeni baada ya kukutwa katika ukanda wa video akifanya njama ya kukwamisha uchunguzi mkubwa wa nchi hiyo unaohusu ufisadi.
Katika rikodi ya kanda hizo, ambazo zimetolewa na gazeti moja, waziri wa mipango, Romero Juca, anaonekana akisema kuondolewa madarakani kwa rais Dilma Rousseff, kutazuia kuchunguzwa kwa kampuni ya serikali ambayo ni kubwa katika uzalishaji wa mafuta, Petrobras.
Hata hivyo, bwana Juca amesema kauli yake hiyo imeeleweka vibaya na kwamba anaunga mkono uchunguzi dhidi ya ufisadi.Juca ni mshirika wa karibu wa rais wa mpito Michel Temer.Bwana Juca amesema atakaa pembeni kwa sasa.
"nitawasilisha waraka katika wizara ya umma, nitaongea na rais Temer, nitaomba likizo kutoka wizarani mpaka wizara itakapofanya maamuzi.Katibu wangu wa wizara, Diogo Oliveira, atachukua nafasi yangu katika kipindi ambacho sitakuwepo.
Waziri huyo amekana kufanya kosa lolote pindi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari:"sijafanya kitu chochote kilichozuia uchunguzi kufanyika. Sijawahi kushirikiana na mtu yeyote katika mahakama kuu au katika wizara ya umma ili kujaribu kuingilia kati uchunguzi.
Kwa maana hiyo, mimi nimetulia. Ninachokisema hapa ni muhimu sana kwa nchi ya Brazil ili kuiokoa kutokana na matatizo ya kiuchumi na tatizo la ajira, na vile vile kujua nani anahusika na nani hahusiki."
"sina mpango wa kuachia nafasi yangu, iwapo hivyo ndivyo mnavyofikiria. Sioni sababu yeyote ya kufanya hivyo, sijafanya kitu chochote kibaya cha kunifanya nijiuzulu.Kama ingekuwa nimefanya uhalifu, ningeng'atuka, lakini hali haiko hivyo.Kwa hiyo uamuzi wa mimi kuendelea kuwepo madarakani unabaki mikononi mwa rais.
Kwa upande wake, Dilma Rousseff amesema kanda hizo zinathibitisha kwamba kuondolewa kwake madarakani ni mapinduzi ya kisiasa yaliyolenga kuwalenga vigogo wanaotuhumiwa katika sakata la Petrobras.
No comments:
Post a Comment