Thursday, January 14, 2016

Kisa kipya cha Ebola chaibuka Sierra Leone

Sierra
Image copyrightAFP
Image captionSierra Leone ilitangazwa kutokuwa na Ebola Novemba mwaka jana
Maafisa wa afya nchini Sierra Leone wamethibitisha kwamba mtu mmoja amefariki kutokana na Ebola, muda mfupi baada ya Shirika la Afya Duniani kutangaza kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huo Afrika Magharibi.
Taifa hilo lilitangazwa kuwa huru kutoka kwa Ebola tarehe 7 Novemba mwaka jana, na kanda hiyo yote ikatangwa kuwa huru kutoka kwa virusi hivyo baada ya Liberia kutangazwa kuwa huru Alhamisi.
Lakini baada ya maafisa wa afya kupima mwili wa mtu aliyefariki kaskazini mwa Sierra Leone, imebainika kwamba alifariki kutokana na virusi hivyo, msemaji wa kituo kimoja cha kupima ugonjwa huo ameambia BBC.
Kifo hicho kilitokea mapema wiki hii.
Msemaji huyo Sidi Yahya Tunis ameambia BBC kwamba mgonjwa huyo alifariki katika eneo la Tonkolili.
Alikuwa amesafiri hadi eneo hilo akitokea eneo la Kambia, karibu na mpaka wan chi hiyo na Guinea.
Mwili huo ulipimwa na wataalamu wa afya kutoka Uingereza.
Mwandishi wa BBC aliyeko Freetown Umaru Fofana anasema maafisa wa afya sasa wanatafuta watu wote ambao walikutana na mtu huyo.
Takriban watu 4,000 wamefariki kutokana na Ebola nchini Sierra Leone tangu Desemba 2013. Kwa jumla, watu 11,000 wamefariki kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo Afrika Magahribi.

No comments:

Post a Comment