Rais Buhari kuanzisha uchungunzi mpya kuhusu wasichana waliotekwa.
Rais wa Nigeria Mohammadu Buhari ameahidi kuanzisha uchunguzi mpya kuhusiana na tukio la kutekwa nyara wasichana zaidi ya 200 wa shule ya Chibok katika jimbo la Borno nchini humo na kundi la itikadi kali la Boko Haram. Kauli hiyo ya Rais Buhari inafuatia maandamano yaliyoongozwa na wazazi wapatao 300 na makundi mengine ya wanaharakati katika mji wa Abuja wakiwa wamebeba mabango ya picha zinazoonyesha sura za baadhi ya wasichana hao waliotekwa kabla ya waandamanaji hao kubebwa katika mabasi na kupelekwa kwenda kukutana kwa mazungumzo na Rais Buhari katika makazi yake. Hii ni mara ya kwanza kwa makundi ya waandamanaji hao na makundi mengine yanayoongoza harakati za kushinikiza kurejeshwa kwa wasichana hao wakiwa hai kukutana na Rais Buhari tangu alipotangaza mwezi Desemba ya kuwa kundi hilo la itikadi kali linaonekana kushindwa kimbinu licha ya wachambuzi wa masuala ya kiusalama kuonya kuwa mapambano dhidi ya kundi hilo bado yanahitajika kwa kiwango kikubwa. Rais Buhari aliwaambia waandamanji hao kuwa mshauri wa taifa hilo wa masuala ya kiusalama Babagana Monguno ataunda kamati maalumu kwa ajili ya kuanzisha uchunguzi mpya kuhusiana na kutekwa kwa wasichana hao.
No comments:
Post a Comment