Tuesday, January 5, 2016


Ikulu ya Marekani ya White House, imetangaza hatua za kudhibiti umiliki wa silaha, ambazo zinawataka wauzaji kupata leseni na kuchunguza historia za wanunuzi zaidi - hatua ambazo Rais Barack Obama amesema ziko ndani ya uwezo wake wa utekelezaji pasipo kuidhinishwa na bunge. Ofisi ya Marekani inayoshughulikia vilevi, tumbaku, silaha na vifaa vya miripuko ATF, sasa itawataka wauzaji silaha katika maduka, maonyesho au kwenye mitandao kupata leseni na kufanya ukaguzi. Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kutangazwa hatua hizo, Rais Obama alisema zilikuwa zinaendana na kifungu cha marekebisho ya pili ya katiba ya Marekani, ambacho kinalinda haki ya kumiliki silaha. Hatua ya Obama kulizunguka bunge inatazamiwa kusababisha mjadala mkali wa kisiasa katika taifa hilo ambako suala la umiliki wa silaha limekuwa likizusha mabishano makali. Tayari chama cha Republican kimemtuhumu rais huyo kwa kutumia vibaya madaraka yake.

No comments:

Post a Comment