Tuesday, January 5, 2016

UN yashutumu kuvamiwa kwa ubalozi Iran


SaudiaImage copyrightAFP
Image captionUbalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran ulichomwa na waandamanaji
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu vikali kushambuliwa kwa ubalozi wa Saudi Arabia nchini Iran na waandamanaji waliokasirishwa na kuuawa kwa mhubiri wa Kishia.
Taarifa ya baraza hilo haijazungumzia kutekelezwa kwa hukumu ya kifo dhidi ya mhubiri huyo maarufu, Sheikh Nimr al-Nimr.
Saudi Arabia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran Jumapili baada ya ubalozi wake kuvamiwa na kuchomwa moto.
Jumatatu, naibu waziri mkuu wa Uturuki Numan Kurtulmus alihimiza nchi hizo mbili kutuliza mgogoro huo, ikisema eneo la Mashariki ya Kati tayari limo hatarini ya kulipuka.
Baraza la Usalama la UN, likijibu barua kutoka kwa Saudi Arabia, limeshutumu shambulio hilo la katika ubalozi Tehran pamoja na shambulio katika afisi ya ubalozi wa Saudia Arabia katika jiji jingine la Iran la Mashhad.
Baraza hilo limeitaka Iran kulinda mabalozi na mali ya ubalozi pamoja na wafanyakazi wake “kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa”.
Limetoa wito kwa pande zote mbili “kushauriana na kuchukua hatua za kupunguza wasiwasi katika kanda hiyo”.
Hata hivyo, baraza hilo halijazungumzia hatua ya Saudi Arabia kumuua Sheikh Nimr al-Nimr, mhubiri wa madhehebu ya Shia, aliyeuawa Jumamosi pamoja na watu wengine 46 baada ya kutuhumiwa kutekeleza makosa yanayohusiana na ugaidi.
IranImage copyrightAP
Image captionMaandamano ya kupinga Saudi Arabia yalifanyika maeneo mengi Iran
Akizungumza New York, balozi wa Saudi Arabia katika UN Abdallah al-Mouallimi amesema mzozo wa sasa ungeepukika iwapo Iran ingejiacha “kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, ikiwemo Saudi Arabia”.
Awali, Saudi Arabia imewahi kuituhumu Iran kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu.
Saudi Arabia na Iran ndizo nchi kuu za Kisuni na Kishia mtawalia eneo la Mashariki ya Kati na zimekuwa wapinzani wakuu.
Nchi hizo huunga mkono pande pinzani katika mizozo Syria na Yemen.
NimrImage copyrightAFP
Image captionSheikh al-Nimr aliuawa Jumamosi
Bw Mouallimi amesema juhudi za kutafuta Amani katika mataifa hayo hazifai kuathiriwa na mzozo wa sasa.
Kufuatia mashambulio hayo, nchi kadha washirika wa Saudi Arabia zimekatiza uhusiano na Iran zikiwemo Bahrain na Sudan na Jumuiya ya Milki za Kiarabu (UAE) ambayo imepunguza hadhi ya ujumbe wa kibalozi wa Iran.
Somalia pia imesema inaunga mkono hatua ya Saudi Arabia kuvunja uhusiano na Iran.

No comments:

Post a Comment