Tuesday, January 5, 2016


Image result for saudi arabia
Balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa amesema uamuzi wa nchi hiyo kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran hautaathiri juhudi za amani nchini Syria na Yemen. Balozi Abdallah al-Mouallimi, amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za amani katika mataifa hayo mawili yanayokabiliwa na vita, na kwamba tahudhuria mazungumzo yajayo kuhusu Syria. Kulikuwa na hofu kimataifa kwamba mzozo kati ya mataifa hayo mawili makubwa katika kanda ya Mashariki ya Kati huenda ukakwamisha juhudi za amani nchini Syria na Yemen, na wajumbe wawili wa Umoja wa Mataifa walitumwa mjini Riyadh kusaidia juhudi za kidiplomasia. Balozi Mouallimi aliongea wakati baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likiandaa taarifa kuhusu mzozo huo, uliyoanzishwa na hatua ya Saudi kumnyonga kiongozi wa Kishia Sheikh Nimr al-Nimr. Baraza la usalama limetoa taarifa na kulaani mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Saudi Arabia. Riyadh imetetea mauaji ya Nimr pamoja na wengine 46, na kusema katika barua iliyotumwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, kwamba walitendewa haki bila kujali itikadi au rangi zao.

No comments:

Post a Comment