Thursday, February 11, 2016

Al-Shabab ''lashambulia uwanja wa ndege Somalia''


Image copyrightairport.kiev.ua
Image captionUwanja wa ndege
Wanamgambo wa kiislamu wamefanya mashambulio ya makombora katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
Walioshuhudia wanasema wanamgambo hao walirusha makombora hayo usiku kucha na kuwa milipuko kadhaa ilisikika karibu na uwanja mkuu wa ndege.
Hata hivyo hakuna ripoti yoyote kuhusu majeruhi, lakini ripoti zinasema kuwa safari kadhaa za ndege kuelekea Mogadishu zimefutiliwa mbali.
Uwanja wa ndege wa Mogadishu unalindwa vikali na unakaribiana na kambi ya wanajeshi wa kulinda amani wa muungano wa Afrika nchini Somalia.
Kikosi hicho cha wanajeshi elfu ishirini na mbili wa muungano huo wanaunga mkono serikali ya nchi hiyo katika harakati zake za kupambana na wanamgambo wa kiislamu.
Ofisi za umoja wa mataifa pia ziko katika kambi hiyo sawa na ubalozi wa mataifa ya kigeni.
Kufikia sasa hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini wapiganaji wa Al shabaab walio na uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda, wamefanya mashambulio kadhaa ya mabomu mjini humo.
Wakati huo huo uchunguzi unaendelea kufuatia mlipuko wa bomu katika ndege moja ya abiria iliyotokea tarehe mbili mwezi huu.
Mlipuko huo ulitokea katika ndege inayomilikiwa na shirika la Daalo muda mfupi tu baada ya kuruka kutoka uwanja huo wa ndege wa Mogadishu na kusababisha kifo cha mlipuaji huyo wa kujitolea, hali iliyoilazimisha ndege hiyo kutua kwa dharura.
Watu kum na watano wamekamatwa kuhusiana na shambulizi hilo la Ndege.

No comments:

Post a Comment