Tuesday, February 16, 2016

Chelsea kumkosa Terry ugenini PSG


Image result for JOHN TERRY
Image copyright
Nahodha wa Chelsea John Terry hatacheza mechi ya hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Paris St-Germain Jumanne jioni.
Terry anauguza jeraha kwenye misuli ya paja.
Meneja Guus Hiddink hata hivyo amesema anaamini klabu hiyo inaweza kujimudu bila nahodha huyo.
Beki huyo wa umri wa miaka 35 hakusafiri pamoja na wachezaji hao kuelekea Ufaransa Jumatatu.
Aliumia wakati wa ushindi wa Chelsea wa 5-1 dhidi ya Newcastle Ligi ya Premia Jumamosi.
Terry alifanya mazoezi mepesi Jumatatu lakini hakuweza kujiunga na klabu hiyo safarini kutokana na kile klabu hiyo ilisema ni “tatizo ndogo kwenye misuli ya paja na kano za goti”.
Kiungo wa kati wa Brazil Oscar, ambaye amekuwa akiuguza jeraha pia, atarejea kwenye kikosi cha Guus Hiddink, ambacho pia kinaongezwa nguvu na mabeki chipukizi Matt Miazga na Jake Clarke-Salter.
Mshambuliaji wa Brazil Alexandre Pato pia hakusafiri na timu, huku Mserbia Nemanja Matic pia akiachwa kutokana na marufuku ambayo anaitumikia.
PSG nao watawapokea tena Zlatan Ibrahimovic, Thiago Motta na Thiago Silva, ambao walipumzishwa wikendi dhidi ya Lille. Mechi hiyo iliisha sare 0-0.
Hata hivyo mabingwa hao wa Ufaransa watamkosa mchezaji wa Ivory Coast Serge Aurier, ambaye amesimamishwa kucheza na klabu hiyo baada ya kutoa matamshi ya chuki dhidi ya meneja wa klabu Laurent Blanc.

No comments:

Post a Comment