Thursday, February 18, 2016

Phiri atabiri ugumu mechi Mbeya City.


KOCHA Mkuu wa Mbeya City Fc, Kinnah phiri amesema ameutabiria mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yake na Azam Fc uliopangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kuwa mgumu na wa kusisimua.
Akizungumza na gazeti hili jana, Phiri alisema matokeo aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans ya mabao 5-1 ni dhahiri yatasababisha mchezo wa Azam kuwa mgumu hasa ikizingatiwa kuwa wapinzani hao wametoka kufungwa na Coastal Union bao 1-0.
“Nafahamu kuhusu matokeo ya Azam Fc kwenye mchezo wao uliopita, hilo litafanya mchezo wetu wa Jumamosi kuwa mgumu ingawa sina shaka sana na hilo, tumetoka kushinda dhidi ya Toto Africans bado tuna ari kubwa kikosini, vijana wangu wako tayari kuwakabili wapinzani wetu, nina uhakika tutashinda,” alisema.
Kuhusu majeruhi kikosini, Phiri aliweka wazi kuwa golikipa Hannington Kalyesubula tayari ameanza mazoezi, pia mshambuliaji Abdalah Juma amerejea kikosini hivyo ana nguvu ya kutosha kupambana na Azam Fc.
City inakutana na Azam Fc kwa mchezo wa Jumamosi ikiwa kwenye nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi na kibindoni ikiwa imekusanya pointi 21, huku timu hiyo ya Azam ikiwa kwenye nafasi ya 3 na pointi 42 mfukoni, ikiwa imecheza michezo 17 tofauti na City yenye michezo 19.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa ni kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Chamanzi Complex ambapo Azam Fc ilifanikiwa kushinda kwa bao mabao 2-1 yaliyofungwa na Mudathir Yahya na Kipre Tchetche huku lile la City likifungwa na Raphael Daud.

No comments:

Post a Comment