Morales ashindwa katika kura ya maoni.
Rais wa Bolivia Evo Morales ameshindwa katika juhudi zake za kutaka muhula wa nne madarakani, ikiwa ni kushindwa kwake kwa mara ya kwanza katika uchaguzi tangu kuingia madarakani mwaka 2006.
Morales mwenye umri wa miaka 56, amekuwa madarakani kwa muongo mmoja, akiungwa mkono zaidi na makundi ya wazalendo pamoja na matawi ya vijijini katika nchi hiyo masikini zaidi katika bara la Amerika.
Wakati akikataa kukubali matokeo hadi mwisho, Morales ameahidi kuheshimu matokeo rasmi baada ya uchaguzi wa hapo Jumapili kuhusiana na mabadiliko katika katiba ambayo yangemruhusu kugombea tena na kurefusha utawala wake hadi miaka 19. Kipindi chake cha sasa cha utawala kinamalizika mwaka 2020.
Wakati asilimia 99.72 za kura zimekwisha hesabiwa , rais wa tume ya uchaguzi Katia Uriona amesema kwamba asilimia 51.3 ya wapiga kura wamesema hapana katika kura hiyo ya maoni, dhidi ya asilimia 48.7 ambao wamesema ndio.
No comments:
Post a Comment