Azam itakaa sawa Ligi Kuu -Kocha.
KOCHA Mkuu wa Azam, Stewart Hall amesema anaamini timu yake itakaa sawa na kurejea kwenye hali ya ushindi.
Azam iliyoanza vizuri msimu wa Ligi Kuu imebadilika kwa siku za karibuni na wiki iliyopita ilipoteza mechi baada ya kufungwa bao 1-0 na Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Timu hiyo imepata kipigo hicho siku chache baada ya kutoka Zambia ilipokwenda kucheza michuano maalumu na kufanya vizuri.
Kipigo cha Coastal kimeiacha Azam kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 42, lakini ikiwa pungufu ya michezo miwili.
Yanga inayoshika nafasi ya pili ina pointi 43 na imecheza mechi 18 na Simba inaongoza msimamo ikiwa na pointi 45 na imecheza mechi 19. Akizungumza na gazeti hili jana, Hall alisema anapambana kurudisha makali ya kikosi chake baada ya kuona kinabadilika siku hadi siku.
“Timu yangu imebadilika kiasi lakini ni kawaida kwenye mpira kuna mambo mengi uchovu, majeruhi na vitu kama hivyo, yapo baadhi ya mambo natakiwa kuyafanyia kazi na nimeshaanza kufanya hivyo,” alisema.
“Tutarudi sawa kwani bado tupo kwenye ushindani wa taji hatupo vibaya, tunaimani tutashinda mechi zetu zijazo bila shaka,” alisema.
Azam inatarajiwa kucheza na Mbeya City ugenini uwanja wa Sokine Mbeya mwishoni mwa wiki hii.
Mechi na City inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute baada ya kuonekana kuzinduka tangu kuwasili kwa kocha mpya Mmalawi Kinnah Phiri ambaye ameahidi kuishushia kipigo Azam.
No comments:
Post a Comment