APANDISHWA KORTINI KWA KUAJIRI WAKONGO.
MKURUGENZI wa bendi ya Kalunde, Deogratius Mwanambilimbi (43) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kuwaajiri na kuwahifadhi wanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo kinyume cha sheria.
Mwanambilimbi alifikishwa mahakamani hapo jana pamoja na wanamuziki watatu wa bendi hiyo, Alain Mulumba (39), Michael Mwenabuntu (33) na Basizi Fayed (27), wanaodaiwa kuishi nchini na kufanya kazi bila kibali.
Akisoma mashitaka, Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma alidai, Februari 10, mwaka huu katika hoteli ya Giraffe Ocean View iliyopo Mbezi Beach, Mulumba, Mwenabuntu na Fayed wakiwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walikutwa wakiishi nchini bila kibali.
Aliendelea kudai kuwa, siku hiyo hiyo katika hoteli hiyo, Mulumba, Mwenabuntu na Fayed walikutwa wakijishughulisha na muziki katika bendi ya Kalunde bila kuwa na kibali cha kufanya kazi nchini.
Katika mashitaka manne yanayomkabili, Mwanambilimbi, Wakili Kagoma alidai huku akijua wanamuziki hao hawana kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini, aliwaajiri katika bendi ya Kalunde na kuwahifadhi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya Uhamiaji.
Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kesi ipangiwe tarehe nyingine kwaajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.
Mwanambilimbi aliachiwa kwa dhamana baada ya kupata mdhamini mmoja kutoka taasisi ya serikali, aliyesaini hati ya Sh milioni 1, pia aliwasilisha hati yake yakusafiria mahakamani. Washitakiwa wengine walirudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini.
No comments:
Post a Comment