Monday, February 22, 2016

ZEC: Hakuna aliyejiondoa rasmi uchaguzi wa Machi.


Maalim Seif
Image captionMgombea urais wa CUF Maalim Seif Hamad amesema hatashiriki uchaguzi huo wa marudio
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha amesema tume yake bado inahesabu vyama vyote kama washiriki katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika 20 Machi.
Hii ni licha ya vyama saba vikiongozwa na Chama cha Wananchi (CUF) kutangaza hadharani kwamba vitasusia uchaguzi huo.
Bw Jecha amesema vyama hivyo havikufuata utaratibu uliowekwa kisheria katika kujiondoa. Baadhi vimetangaza tu kupitia vyombo vya habari.
“Mgombea urais wa CUF na wagombea wa chama hicho wa viti vya uwakilishi na udiwani, na vyama vingine sita wameandikia ZEC wakisema hawatashiriki,” amesema kupitia taarifa.
“Lakini wagombea hao wote na vyama husika hawajafuata utaratibu ufaao. Mpaka tunapowasilisha taarifa hii, hakuna chama hata kimoja kati ya vyama ambavyo vimejinadi kuwa havitashiriki katika uchaguzi kilichoiandikia Tume kuwa kimefuta udhamini wa wagombea wake kushiriki katika uchaguzi," amesema Bw Jecha
"Utaratibu wa kujitoa kwa wagombea katika uchaguzi umefafanuliwa vizuri sana katika kanuni ya uchaguzi ya mwaka 2015."
Kwa mujibu wa Bw Jecha, ni wajibu wa chama kuandikia ZEC na kuwaondoa wagombea urais ambao chama hicho kinawadhamini.
Be Jecha mesema vyama husika, CUF ikiwemo, havijafanya hilo.
Mgombea pia anaweza kujiondoa kwa kutoa taarifa ya maandishi aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa mwenyekiti si zaidi ya saa 10 jioni siku ya uteuzi lakini taarifa hiyo inafaa iambatanishwe na tamko la kisheria lililotolewa.
Uchaguzi
Image captionChama cha CUF kimetangaza kwamba hakitashiriki uchaguzi wa marudio
Tamko hilo la kisheria linafaa kutiwa saini na mgombea mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kwa mgombea wa urais na hakimu kwa mgombea wa uwakilishi au udiwani, mambo ambayo hayakufanyika, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi.
“Ni muhimu sana kufahamu na kufuata sheria zinazosimamia uchaguzi,” amesema.
Kwa mujibu wa Bw Jecha, tume inaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo na karibuni wagombea wote wa urais watapewa ulinzi na tume hadi matokeo yatangazwe.
Vyama ambavyo vimethibitisha kushiriki, kwa mujibu wa ZEC ni CCM, ACT, ADC CCK AFP, SAU, TLP na ADA-TADEA.
Uchaguzi visiwani Zanzibar unarudiwa baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
Tume ilifuta matokeo hayo ikisema kulikuwa na kasoro nyingi.

No comments:

Post a Comment