Monday, February 22, 2016


Rais wa Uganda Yoweri Museveni amepuuzilia mbali ukosoaji wa Umoja wa Ulaya na Marekani kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo Alhamisi wiki iliyopita. Akizungumza nyumbani kwake huko Kiruhura kusini magharibi mwa Uganda hapo jana, Museveni aliwaambia waangalizi wa kigeni wasimwambie cha kufanya kupitia mihadhara asiyoihitaji kutoka kwa mtu yeyote. Tume ya waangalizi ya Umoja wa Ulaya ilisema uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya hofu, huku mkuu wa tume hiyo Eduard Kukan akisema ulivurugwa na ukosefu wa uwazi na uhuru katika tume ya uchaguzi. Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986 alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo Jumamosi iliyopita. Mpinzani mkuu wa rais Museveni, Dokta Kizza Besigye alisema uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu. Besigye, ambaye anazuiliwa nyumbani kwake, amewatolea wito wafuasi wake waandamane ili aachiwe huru.

No comments:

Post a Comment