Wednesday, February 17, 2016

Jonisia Rukiyaa kuchezesha mechi kati ya simba na yanga .
Image result for TFF
MWAMUZI wakike Jumamosi atapuliza filimbi kuchezesha pambano la Simba na Yanga litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku kiingilio cha chini kikiwa ni sh 7,000.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana lilimtangaza Jonisia Rukiyaa kutoka Kagera kuwa mwamuzi wa kati atakayeamua pambano hilo la watani wa jadi ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa.
Msemaji wa TFF Baraka Kizuguto aliwataja waamuzi wa saidizi katika pambano hilo kuwa ni wasaidizi ni Josephat Bulali kutoka Tanga, Samweli Mpenzu kutoka Arusha, mwamuzi wa akiba Elly Sasii wa Dar es Salaam na Kamishna ni Khalid Bitebo wa Mwanza.
Bulali alikuwa kati ya waamuzi wawili wasaidizi wakati Rukiya alipochezesha pambano la Yanga na Simba katika Bonanza la Nani Mtani Jembe, ambalo Simba iliitwanga Yanga mabao 2-0.
Kiingilio cha chini katika pambano hilo kitakuwa Sh 7,000 huku kile cha juu kabisa ni 30,000, huku viingilio vingine vitakuwa ni Sh 20,000 na 10,000.
“Tiketi zitauzwa kuanzia Ijumaa katika maeneo ambayo yamekuwa yakitumika kuuzia, kwa hiyo tunaomba watu wanunue mapema ili kuepuka usumbufu wa kuuziwa tiketi feki,” alisema.
Kuelekea kwenye pambano hilo la jadi, timu zote mbili zinaendelea na kambi katika maeneo tofauti huku kila mmoja akimtambia mwenzake kushinda.
Yanga imeweka kambi Pemba kwa maandalizi ya mechi hiyo na Simba ikijichimbia Morogoro, yote ni kuhakikisha wanajiandaa vyema kupata pointi tatu na kuvunja rekodi ya mwenzake.
Kabla ya pambano hilo, Simba inaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 45 wakati Yanga iko katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 43 lakini imecheza mechi pungufu ya Simba.
Mbali na mechi ya Simba na Yanga, michezo mingine itakayochezwa siku hiyo kwenye viwanja tofauti ni Mbeya City dhidi ya Azam (Sokoine), Stand United v JKT Ruvu (Kambarage), Toto Africans dhidi ya Kagera Sugar (CCM Kirumba), Mgambo Shooting dhidi ya Tanzania Prisons (Mkwakwani) na Majimaji FC dhidi ya Mtibwa Sugar (Majimaji).
Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa michezo miwili, Mwadui FC v Coastal Union uwanja wa Mwadui Complex, huku Ndanda FC wakicheza dhidi ya African Sports uwanja wa Nagwanda Sijaona mjini Mtwara.

No comments:

Post a Comment