Tuesday, November 24, 2015

Magufuli aamua sikukuu iwe siku ya kazi

Sherehe
Sherehe ya Uhuru itaadhimishwa kama kawaida kuanzia mwaka ujao
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ameamua hakutakuwa na sherehe za kuadhimisha Siku ya Uhuru mwezi ujao na badala yake akasema itumiwe kufanya kazi.
Sherehe hiyo huadhimishwa kila Desemba 9.
Hatua hii ni moja ya mambo yasiyo ya kawaida ambayo kiongozi huyo ameyafanya katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja tangu kuchukua ungozi.
“Maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu 2015 yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi -Uhuru na Kazi - katika Taifa letu,” ilisema taarifa iliyotumwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya ikulu Gerson Msigwa hapo jana.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.”
Taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli ametumia Sheria ya Sikukuu za Kitaifapamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko.”
Rais alisema kadhalika alisema hatua hiyo italiokolea taifa pesa nyingi ambazo hutumiwa katika maandalizi na kufanikisha sherehe hizo.
“Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua,” amesema.
Hata hivyo aliongeza kuwa sherehe hizo zitaendelea kuadhimisha kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka ujao.
Miongoni mwa mambo aliyoyafanya Rais Magufuli ni kufanya ziara za kushtukiza Hazina Kuu na Hospitali ya Muhimbili, kuweka masharti kwa safari za nje za maafisa wa serikali.
Aidha, aliamua fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge zipelekwe katika hospitali ya taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda na magodoro ya wagonjwa wanaolala chini limetekelezwa.
Wadau mbalimbali walichanga fedha kiasi cha shilingi milioni 225 lakini Dkt Magufuli aliagiza fedha za kutumiwa zisizidi shilingi milioni 15 na masalio yapelekwe hospitali ya Muhimbili.

No comments:

Post a Comment