Ubelgiji yashauri raia wake waondoke Burundi
Ubelgiji
imewashauri raia wake kuondoka Burundi, huku Muungano wa Ulaya nao
ukipunguza maafisa wake wanaohudumu huko kutokana na kuongezeka kwa
machafuko.
Balozi wa EU nchini humo Patrick Spirlet amesema hatari ya kutokea mapigano zaidi imeongezeka.
Hayo
yamejiri huku idara ya Amani ya Usalama ya Muungano wa Afrika
ikikutana mjini Addis Ababa kujadili mpango wa kutuma walinda amani
nchini humo.
Kamishna wa Amani wa AU Smail Chergui amesema atatuma
maafisa nchini Uganda kuandaa mazungumzo kati ya Rais Nkurunziza na
upinzani.
Watu zaidi ya 200 wameuawa tangu Aprili Rais Nkurunziza
alipotangaza kuwa angewania urais kwa muhula wa tatu. Alishinda uchaguzi
mwezi Julai.
Mnamo Alhamisi, Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa kwa kauli moja lilipitisha azimio lenye mapendekezo mengi
yakiwemo uwezekano wa kutumwa kwa walinda Amani, na kuwekwa kwa vikwazo.
Kiongozi mmoja wa upinzani nchini Burundi tayari ameuhimiza Umoja wa Mataifa kutuma walinda usalama nchini humo.
Charles
Nditije, mkuu wa kundi la upinzani la UPRONA, ameambia shirika la
habari la Reuters kwamba wanafurahishwa na juhudi za UN kuhimiza
mashauriano lakini wamevunjwa moyo na kutoumwa kwa walinda Amani na
kutoafikiwa kwa maelewano kuhusu vikwazo.
No comments:
Post a Comment