Thursday, December 31, 2015


Kiasi cha watu 16 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa na miripuko iliyotokea jana kwenye migahawa mitatu kaskazini mashariki mwa Syria. Mkurugenzi wa shirika linalofatilia haki za binaadamu lenye makao yake Uingereza, Rami Abdel Rahman, amesema mripuko mmoja uliotokea kwenye mji wa Qamishli, ulisababishwa na mripuaji aliyejitoa muhanga. Shirika la habari la Amaq linalowaunga mkono wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu-IS, limesema kundi hilo limedai kuhusika na mashambulizi kwenye mji huo, ambao uko karibu na mpaka wa Uturuki na karibu na Iraq. Mji wa Qamishli uko chini ya udhibiti wa pamoja wa serikali ya Syria na uongozi wa Kikurdi, ambao wametangaza maeneo ya ''uhuru wa kujitawala'' kuzunguka maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Syria. Kwa mujibu wa shirika hilo, miripuko yote katika migahawa mitatu imetokea kwenye eneo linalodhibitiwa na vikosi vya serikali.

No comments:

Post a Comment