Sunday, December 20, 2015



Rwanda yaunga mkono mabadiliko ya katiba.


Rwanda imepiga kura kwa wingi kuunga mkono mabadiliko ya katiba yatakayomruhusu Rais Paul Kagame kutawala hadi mwaka 2034. Maafisa wa uchaguzi wamesema jana wakizingatia matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa nchi nzima. Kwa mujibu wa kura zilizohesabiwa katika wilaya 30 za Rwanda pamoja na kura za nchi za nje, kura ya ''Ndiyo'' inayounga mkono kubadilishwa kwa katiba imepata asilimia 98.4, huku asilimia 1.6 ya wapiga kura wakipinga. Hata hivyo, tume ya uchaguzi imesema hayo bado ni matokeo ya awali. Rais Kagame, mwenye umri wa miaka 58, sasa anaweza kutawala kwa miaka mingine 17. Mabadiliko hayo yanamruhusu Rais Kagame kugombea kwa awamu ya tatu ya kipindi cha miaka saba mwaka 2017 na wakati sheria mpya itakapoanza kutumika ataweza kugombea tena kwa vipindi vingine viwili vya miaka mitano.

No comments:

Post a Comment