Monday, December 14, 2015

Raia wa Marekani kuondoka Burundi



Serikali ya Marekani imeshauri Raia wake walio nchini Burundi kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo baada ya watu 87 kuuawa kwenye ghasia zilizotokea siku ya Ijumaa.
Ghasia zilizojitokeza kwenye mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura ni mbaya zaidi tangu kuanza kwa vurugu mwezi Aprili baada ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania tena urais kwa muhula wa tatu.
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya Ijumaa.
Mwezi uliopita, Ubelgiji pia iliwashauri raia wake kuondoka Burundi, huku Muungano wa Ulaya (EU) nao ukipunguza wahudumu wake, kwa kuondoa wafanyakazi ambao ni wa muda, "familia na wafanyakazi ambao si muhimu sana."
"Kufuatia machafuko ambayo yanaendelea kuongezeka, Wizara ya Kigeni imeagiza kuondoka kwa jamaa za maafisa wa Marekani na maafisa ambao si wa kushughulikia dharura nchini Burundi," taarifa ya Marekani ilisema.
"Ubalozi wa Marekani unaweza kutoa huduma za dharura kwa kiwango cha chini tu kwa raia wake nchini Burundi."

No comments:

Post a Comment