Friday, December 11, 2015

Mashirika yasitisha safari za ndege Burundi

Burundi

Watu wenye silaha wanaripotiwa kushambulia kambi na chuo cha jeshi
Mashirika ya ndege ya Kenya Airways na RwandAir yamesitisha safari zake za kuelekea mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, kufuatia makabiliano ya risasi mjini humo.
Kwa mujibu wa afisa mkuu wa mawasiliano wa shirika la ndege la Kenya, KQ, Wanjiku Mugo, safari hizo zimesitishwa kutokana na ukosefu wa wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa Bujumbura.
Serikali ya Burundi imesema uwanja huo haujafungwa ila tu shughuli zimetatizika kwa sababu wafanyakazi hawakuweza kufika katika uwanja huo, kutokana na makabiliano makali ya risasi kati ya wapinzani wa serikali walioakuwa wamejaribu kuvamia kambi kadhaa za kijeshi mjini humo.
Shirika la kimataifa ya Msalaba mwekundu ICRC nalo kwenye Twitter limesema kuwa halikufanikiwa kuingia katikati mwa mji mkuu Bujumbura kutokana na vizuizi vilivyowekwa na maafisa wa jeshi ambao wanaendelea na msako dhidi ya watu wanaomiliki silaha.
Ripoti zinasema kuwa watu wanane wameuawa kwenye makabiliano hayo huku wengine wengi nao wakiwa wamejeruhiwa.
Mitaa ya Mutakula na Musaga ndiyo iliyoathirika zaidi huku wakaazi wa mitaa hiyo wakirpoti milio ya risasi kuanzia saa kumi alfajiri.
Huku hayo yakijiri Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza ameongoza mkutano wa baraza lake la mawaziri.

No comments:

Post a Comment