Sunday, December 13, 2015

Mapigano yazuka upya C.A.R


Mapigano yamezuka katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Bangui.
Duru zinasema kuwa mapigano hayo yametibuka katika vitongoji vya Gobongo mapema leo kabla ya wenyeji kutoka makwao kujitokeza kushiriki katika kura ya maoni.
Yamkini watu 5 wameripotiwa kujeruhiwa katika makabiliano kati ya watu wanaopinga zoezi la kupiga kura ya maoni kuhusu pendekezo la kubadilisha katiba ya nchi hiyo iliyosakamwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Aidha kumeripotiwa mlipuko wa guruneti na ufyatulianaji wa risasi katika kitongoji cha Gobongo.
Serikali ya mpwito imekuweko tangu rais Francois Bozize kung'olewa madarakani na wapiganaji wa Seleka mwaka wa 2013.

Shuguli ya upigaji kura ulitatizika katika maeneo mengi hususan visa vya utovu wa usalama ukishuhudiwa.
Aidha wapigaji kura katika eneo la Bosangoa walilazimika kukimbilia usalama wao kufuatia ufyatulianaji wa risasi.
Bosangoa, ndiko anakotokea rais wa zamani wa taifa hilo Francois Bozize.
Bozize hatashiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Eneo lingine lililoathirika na makabiliano hayo ni Kaga-Bandoro, iliyoko Kaskazini mwa taifa hilo.
Katika eneo hilo karatasi na vifaa vya kupigia kura viliteketezwa moto.

Eneo la Kaga-Bandoro, ndiko anakotokea kiongozi wa zamani wa Seleka.
Endapo raia watakubali kufanyike mabadiliko ya kikatiba, basi bunge la juu ama Seneti litaundwa ilikulinda uhuru wa kila mtu wa kuabudu.
Takriban watu milioni mbili wanatarajiwa kushiriki katika kura ya maoni ya kutekeleza mabadiliko ya katiba.
Uchaguzi mkuu umeratibiwa kufanyika Desemba tarehe 27.

No comments:

Post a Comment