Mhubiri wa Canada afungwa maisha Korea Kaskazini
Mahakama ya juu zaidi Korea Kaskazini imemhukumu mhubiri kutoka Canada kifungo cha maisha jela na kazi ngumu.
Hyeon Soo Lim, 60, aliyekamatwa mjini Pyongyang baada ya kuzuru taifa hilo Januari kwa kazi ya kibinadamu amehukumiwa kwa makosa ya “uhalifu dhidi ya dola.”
Bw Lim, ambaye ni kiongozi wa Light Korean Presbyterian Church, alikuwa ameenda kusaidia kituo cha kutunza wagonjwa, kituo cha kuwatunza watoto na kituo cha kutunza mayatima.
Mhubiri huyo kutoka Korea, anadaiwa kukiri kuhusika katika njama ya kupanga kupindua serikali na kuunda taifa la kidini.
Shughuli zozote za kidini ni marufuku nchini Korea Kaskazini.
Taifa hilo mara kwa mara huwakamata na kuwazuia wageni wanaoenda huko kwa shughuli za kidini au kimishenari.
Bw Lim alihukumiwa baada ya kesi yake kuendeshwa kwa muda mfupi na mahakama ya juu ya Korea Kaskazini.
Inadaiwa mhubiri huyo amekiri kutoa mihadhara na kusema “Korea Kaskazini inafaa kusambaratishwa na mapenzi ya Mungu”, na kusaidia Marekani na Korea Kusini kutoa usaidizi kwa wanaotoroka Korea Kaskazini.
No comments:
Post a Comment