Jeshi la Nigeria labomoa madhabahu ya kishia
Kundi kuu la kiislamu nchini Nigeria linaloungwa mkono na waislamu wa Kishia wa Iran, linasema kuwa mke wa kiongozi mkuu Sheikh Ibrahim Zakzaky, ameuwawa katika makabiliano na jeshi kaskazini mwa mji wa Zaria.
Vuguvugu la kiislamu nchini Nigeria (IMN) linadai kuwa Zeenat Ibraheem ameuwawa kwa pamoja na mwanaye Sayyid Ibraheem Zakzaky.
Sheikh Zakzaky alikamatwa na wanajeshi waliozingira nyumba yao kufuatia madai kuwa wanachama wa kundi hilo walijaribu kumuua kamanda mkuu wa jeshi Jenerali Tukur Buratai huko Zaria siku ya Jumamosi.
Hata hivyo, kundi la IMN limekanusha madai hayo na kulaumu jeshi kwa kuwauwa zaidi ya wanachama 20 wa kundi hilo, katika makabiliano makali huko Zaria.
Vuguvugu hilo la kiislamu nchini Nigeria linapinga kundi la jihad la waislamu Wa-Sunni la Boko Haram, lakini limekuwa likikabiliana mara kwa mara na jeshi la taifa hilo.
Wakati huohuo, wanajeshi wa Nigeria wanaendelea na mashambulizi yao dhidi ya dhehebu hilo la kishia kwa siku ya 3 mfululizo.
Ripoti zinasema kuwa madhabahu makubwa zaidi ya dhehebu hilo la kishia yameharibiwa na wanajeshi hao.
Aidha nyumba ya kiongozi wa kishia nchini Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky imebomolewa.
Jeshi halijajibu madai dhidi yake.
No comments:
Post a Comment