Saturday, December 26, 2015

Kiongozi wa kundi la waasi auawa Syria


JayshImage copyrightAFP
Image captionAlloush ndiye aliyeanzisha kundi la Jaysh al-Islam
Kiongozi mkuu wa kundi la waasi la Jaysh al-Islam, moja ya makundi yenye nguvu zaidi Syria, ameuawa kwenye shambulio la makombora.
Zahroun Alloush, 44, ambaye ndiye mwanzilishi wa kundi hilo aliuawa kwenye shambulio la makombora mashariki mwa Damascus alipokuwa kwenye mkutano.
Aliuawa pamoja na viongozi wengine wa kundi hilo, habari ambazo zimethibitishwa na makundi ya waasi na jeshi la Syria.
UrusiImage copyrightGetty
Image captionUrusi na Syria zilikataa kutambua mkutano huo wa waasi Saudi Arabia
Kundi hilo linaloungwa mkono na Saudi Arabia ni moja ya makundi makubwa ya waasi wanaopigana na Rais Bashar Assad na ngome yake ni maeneo ya Ghouta, mashariki mwa nchi hiyo.
Majuzi lilihudhuria mkutano mkuu wa wapinzani wa Bw Assad mjini Riyadh, mkutano ambao ulijadili mkakati wa mazungumzo ya Amani na serikali.
Makombora kumi yanadaiwa kuanguka eneo ambalo makamanda wa Jaysh al-Islam walikuwa mkutanoni, kwa mujibu wa runinga ya al-Arabiya inayofadhiliwa na serikali ya Saudi Arabia.
Naibu kiongozi wa kundi hilo pia aliuawa.
JayshImage copyrightReuters
Image captionKundi la Jaysh al-Islam limekuwa likipigana katika mji wa Damascus
Jaysh al-Islam baadaye walimteua Issam al-Buwaydani – ajulikanaye pia kama Abu Humam – kuwa kiongozi wake mpya.
Bw al-Buwaydani anatoka mji wa Douma, mashariki mwa Damascus.
Jeshi la Syria, kupitia taarifa kwenye runinga ya taifa, limesema ndilo lililotekeleza shambulio hilo lakini baadhi ya wanaharakati wanasema lilitekelezwa na Urusi.
Duru nyingine zimedokeza huenda jeshi la Syria lilitekeleza shambulio hilo likitumia makombora ya Urusi.
Urusi, ambayo ni mshirika mkuu wa Rais Assad, imekuwa ikitekeleza mashambulio ya angani dhidi ya wapinzani wa Bw Assad tangu mwisho wa Septemba.

No comments:

Post a Comment