Thursday, December 3, 2015

Uingereza yashambulia Islamic State Syria

 Tornado
 Ndege aina ya Tornado zilishambulia IS muda mfupi baada ya mashambulio kuidhinishwa
Ndege za kijeshi za Uingereza zimetekeleza mashambulio ya angani dhidi ya kundi la Islamic State nchini Syria saa chache baada ya bunge kuidhinisha mashambulio hayo, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imethibitisha.
Duru za serikali zimesema ndege hizo tayari zimerejea kambini katika visiwa vya Cyprus.
"Shambulio limetekelezwa Syria,” mdokezi huyo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Awali, wabunge nchini Uingereza walikuwa wamepiga kura kwa wingi kuunga mkono mashambulio hayo, wabunge 397 wakiunga mkono dhidi ya 223, baada ya mjadala mkali uliodumu saa 10 katika bunge la Commons.
Jumla ya wabunge 66 wa chama cha Labour waliunga mkono serikali huku David Cameron akipiata kura nyingi kuliko ilivyotarajiwa katika bunge hilo.
 
 
Cameron alisema mashambulio hayo yanahitajika kuliweka taifa salama
Waziri Mkuu huyo alisema amechukua “hatua ifaayo kuweka taifa salama” lakini wapinzani wake walisema hilo ni kosa.
Ndege nne za kijeshi ziliripotiwa kupaa kutoka kambi ya kijeshi ya RAF Akrotiri, Cyprus, baada ya kura hiyo kupigwa.
Ndege nyingine nne zilikuwa tayari kupaa kutoka kambi hiyo, ambayo imekuwa ikitumiwa kutekeleza mashambulio nchini Iraq.
Mbili kati ya ndege hizo nne aina ya Tornado zilirejea Cyprus saa tatu baadaye, muda mfupi baada ya saa 03:00 GMT.
 
Kabla ya kura kupigwa, baadhi ya wanaharakati waliandamana London kupinga vita hivyo
Mwandishi wa BBC anayeangazia masuala ya ulinzi Jonathan Beale alisema ndege hizo ziliondoka RAF Akrotiri zikiwa na mabomu ya uzani wa 500lb aina ya Paveway na kurejea bila mabomu hayo.
Mwandishi wa BBC anayeangazia masuala ya kisiasa amesema jeshi la wanahewa la Uingereza, maarufu kama RAF, “limekuwa likijiandaa kuhusika katika mashambulio hayo, kujiunga na mataifa mengine ya muungano yanayokabiliana na IS nchini Syria, “kwa miezi kadha”.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Jeremy Corbyn alipinga mashambulio hayo lakini chama chake kiligawanyika, baadhi ya viongozi wake wakuu wakijitenga na msimamo wake.

No comments:

Post a Comment