Mwanahabari aliyekamatwa Kenya aachiliwa
John Ngirachu Facebook
Mwanahabari mmoja
mashuhuri nchini Kenya aliyekuwa amekamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa
usalama Kenya baada ya kudaiwa kuchapisha habari kuhusu tuhuma za
ufisadi serikalini ameachiliwa huru.
Mwanahabari huyo John
Ngirachu wa shirika la habari la Nation Media Group ameachiliwa baada ya
kuandikisha taarifa na maafisa wa uchunguzi wa jinai akiwa ameandamana
na mawakili wake wawili.
Bw Ngirachu, ambaye ni mhariri
anayeangazia habari za bunge, anadaiwa kuandika taarifa iliyonukuu
habari kutoka kwa kikao cha faraghani cha Kamati ya Bunge kwenye gazeti
la Daily Nation.
Habari hizo zinahusu ufisadi katika Wizara ya Usalama na Masuala ya Ndani kuhusu matumizi ya Sh3.5 bilioni pesa za Kenya.
Waziri
wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery, anasema aliwasilisha habari hizo
faraghani na anasema yeyote aliyefichua habari hizo sharti aeleze
alizitoa wapi.
“Kama waziri anayesimamia usalama, nachukulia hatua
hii kama njama ya kudhuru taifa, kuhujumu juhudi za kudumisha usalama
na kuonyesha wizara hii kama fisadi na isiyofuata sheria.
"Haikubaliki,” alisema Nkaissery kwenye kikao na wanahabari siku moja baada ya kuchapishwa kwa habari hizo.
Lakini mmoja wa wahariri wakuu wa shirika la habari la Nation Media, Linus Kaikai amekanusha madai hayo
“Hatujakiuka maadili yoyote, vikao vya bungeni wazi na katika katiba tunaruhusiwa kuwa katika vikao vile’’.
"Habari hizo zilijulikana Nkaissery alipofika katika kikao hicho cha kamati ya bunge,” Bw Linus Kaikai ameiambia BBC.
“Kwa sasa mawakili wetu wanashughulika kujaribu kumtoa korokoroni’’.
‘’Kwa sasa kile tunajali zaidi ni uhuru wa Ngirachu.”
Bw Ngirachu, aliandika mara ya kwanza kwenye mtandao
wake wa Twitter Novemba 5 akidai kuandamwa na afisa wa uchungzi wa
jinai aliyemtaka "aeleze alikotoa habari hizo”.
"Afisa wa CID
anapigia simu wanahabari wote walioandika kuhusu maswali ya Mkaguzi Mkuu
wa hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya Sh3.8 bilioni katika wizara ya
masuala ya ndani,” aliandika.
Kwa mujibu wa Bw Ngirachu, habari hizo zilitolewa kwenye kikao cha Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC).
Watumiaji
wa mtandao wa Twitter wamekuwa wakieleza kukasirishwa kwao na kukamatwa
kwa mwanahabari huo, wakitumia kitambulisha mada #FreeNgirachu, yaani
mwachilie huru Ngirachu.
Kiongozi wa Muungano wa upinzani CORD
Raila Odinga pia ametoa taarifa akishutumu kukamatwa kwa mwanahabari
huyo na kuitaka serikali imwachilie huru mara moja.
Waandishi wa habari wanapanga kuandamana hapo kesho ili kupinga kukamatwa kwake na kuishinikiza serikali kumuachilia huru.
Aidha shirika la wanahabari wanapanga kuwasilisha kesi mahakamani ya kutaka aachiliwe huru.
No comments:
Post a Comment